Tuesday, August 9, 2011

Wenye Saluni Dar Walia na Mgawo wa Umeme

Wenye Saluni Dar Walia na Mgawo wa Umeme

WAFANYABIASHARA wa saluni jijini Dar es Salaam wamesema mgao wa umeme umewatia hasara kubwa na sasa wanafikiria kufunga biashara zao.

Wamesema mgao huo unasababisha hasara kwao kila siku kutokana na kutofungua saluni zao ambazo wanazilipia kiasi kikubwa cha fedha.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa saluni nyingi za kike na za kiume zimekuwa zikifungwa takribani siku nzima kutokana na mgao wa umeme katika maeneo mbalimbali jijini hapa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, baadhi ya wamiliki wa saluni hizo katika maeneo ya Kimara, Sinza na Buguruni, walisema mgao wa umeme ni kikwazo kikubwa katika biashara yao.

Aisha Abdallah ambaye ni mmiliki wa saluni ya kike ya Baby Beauty saloon iliyopo Kimara Mwisho aliliambia Mwananchi kuwa tangu kuanza kwa mgao wa umeme, amekuwa akifanya kazi siku tatu tu kwa wiki, badala ya siku saba jambo ambalo alisema linanasababisha hasa kubwa kwake.

“Umeme unaniletea hasara kubwa sana, zamani nilikuwa nafanya kazi siku saba na kunifanya nipate fedha za kutosha kuendesha maisha yangu, kulipa kodi ya ofisi hii, lakini sasa hali naona inazidi kuwa mbaya kila kukicha, na mwenye kibanda anadai kodi yake kila mwezi, ni kero tupu” alisema Abdallah.

Alisema umeme katika maeneo hayo unakatika siku nne kuanzia asubuhi na kurudi usiku muda mbao hawezi kupata wateja na hivyo kumfanya ashinde siku nzima bila kuingiza pesa yeyote ile.

“Kawaida kwa siku nilikuwa nikipata Sh 30,000 katika siku za kawaida na Sh 50,000 kwa siku za mwisho wa wiki kiwango ambacho kiliweza kufikia malengo, lakini sasa mambo yameharibika maana nafanya kazi siku mbili au tatu kwa wiki na kufanya mapato yangu yaporomoke kwa zaidi ya asilimia 70”, alisema.


Bibi Harusi akiwa saluni. Shughuli nyingi zinazohusiana
na utengenezaji wa nywele hutegemea nishati ya umeme.

Naye Joel Sandi mmiliki wa saluni ya kiume ya Bon Love ya Sinza alisema kuwa mgao wa umeme umekuwa mwiba mchungu kwao na kwamba saluni zao zimekuwa ni kijiwe cha kupigia soga tu kutokana na kukosa umeme siku nzima.

“Kuna hatari ya kufunga biashara hii, maana uwezo wa kulipa kodi za pango haupo tena, na kama tutaendelea kufanya biashara hii itakuwa ni kwa ajili ya kulipia kodi tu, inakera sana na inabidi serikali ifanye mchakato wa kumaliza tatizo hili mapema,” alisema Sandi.

Alisema pamoja na kwamba baadhi saluni kubwa zinatumia jenereta wakati umeme ukikatika, lakini kwa wafanyabisahara wadogo hilo kwao ni gharama kubwa na kwamba hawawezi kulimudu.

Ni zaidi ya miezi miwili sasa tangu shirika la umeme nchini Tanesco
litangaze uwepo wa mgao wa umeme kwa nchi nzima jambo ambalo limeathiri sekta mbalimbali ikiwemo ya wajasiriamali kama hawa wa saluni.

(Habari hii ni kwa mujibu wa Gazeti Maarufu la Mwananchi)

No comments:

Post a Comment