Friday, August 12, 2011

Je Wajua kuwa machungwa ni zao la matunda linalovunwa sana duniani?

CHUNGWA ni tunda la msimu. Ni kati ya matunda yanayovunwa sana duniani. Jina la kisayansi ni Citrus aurantium L. var. sinensis L. au Citrus sinensis (L.) Osbeck.

Tunda lenyewe ni kijani na rangi inabadilika kuelekea njano likiiva. Pamoja na limau, danzi, balungi na ndimu ni mojawapo kati ya matunda chungwa. Siku hizi ni tunda linalovunwa zaidi kati ya matunda chungwa.

Asili yake ni katika Asia ya Kusini-Mashariki ambako lilioteshwa na wakulima. Kuna aina mbili yanayotofautiana kwa ladha ama chungu au tamu. Lenye ladha chungu liliwahi kusambaa duniani hivyo jina la Kiswahili limetunza ladha hii hata kama matunda mengi yanayopandwa siku hizi ni aina tamu.

Chungwa tamu lilisambaa kote duniani baada ya Wareno kuchukua machipuko yake na kuyapanda kwanza Ureno baadaye hata Amerika na Afrika kuanzia karne ya 15. Chungwa, na hasa chungwa tamu, ni jamii ya matunda ya citrus, na huaminika kuwa yalikuzwa miongoni mwa enzi za pomelo na tangerine.

Mti wake mdogo utoao maua hufikia urefu takribani mita kumi na majani yake yasiyokauka muda wote. Machungwa asili yake ni huko kusini mwa Asia. Tunda lifahamikalo kisayansi kama citrus sinesis huitwa chungwa tamu ili kutofautisha na citrus aurantium, chungwa chungu.

Matunda yote jamii ya jenasi ya citrus, huzaliana na familia yao hujumuisha machungwa, ndimu na limao. Matunda ya jamii hii huonwa kama ni ya aina ya beri sababu ya kuwa na mbegu nyingi, kuwa laini na nyama nyingi huku yakikua kutoka kwenye ovari moja.

Kama ilivyo kwa jamii ya matunda ya citrus, machungwa nayo huwa na hali ya asidi, yenye kiwango cha pH karibu na 2.5 -3, kulingana na umri wake, ukubwa na aina ya chungwa. Japo si kama ilivyo kwa limao, bado machungwa huwa na kiwango cha asidi cha kutosha, sawa kabisa na hata siki ya nyumbani.

Machungwa kwa kawaida hulimwa kwa ajili ya biashara na hulimwa maeneo mengi duniani. Wazalishaji wa machungwa wanaoongoza duniani ni Brazili, Marekani na Meksiko. Machungwa huathirika kwa haraka sana na ukungu hivyo huhitaji matunzo mazuri pindi joto dogo sana linapotegemewa.

Michungwa huweza kukuzwa maeneo yenye joto na hata yale yenye baridi. Kama ilivyo kwa matunda mengine ya citrus, ili kupata mazao mazuri haina budi kukuza michungwa katika joto la nyuzijoto 15.5 °C - 29 °C.

Miti ya machungwa iliooteshwa kutokana na mbegu zilizonunuliwa madukani inaweza kuwa tofauti kabisa na ile miti ya asili iliyozalisha mbegu hizo. Hii hutokana na mabadiliko ya kizazi yanayotokana na kuchanganywa mbegu kisayansi kwa muda mrefu.

Ili kupata mmea wa mchungwa kama tunda ambalo linanunuliwa, huna budi kuitunza mbegu hiyo kwenye unyevunyevu kisha tu baada ya kuzitua kwenye tunda na kuziotesha katika hali ya unyevu; na pindi mmea uchipuapo hapo ukapandwe kwenye udongo kusudiwa.

Machungwa yanakuzwa katika hali mbalimbali za joto duniani kote, na ladha yake hubadilika kuanzia hali ya utamu mpaka uchungu kabisa. Tunda kwa kawaida humenywa na kuliwa au huminywa na sharubati yake kunywewa.

Limezungukwa na ganda lenye ladha chungu lakini huweza kukamuliwa na kuondolewa maji yake na kutumika kwa chakula cha mifugo. Pia, hutumika kuongeza ladha ya vyakula vingine na hata maganda yake hufaa kwa kazi hii.

Sehemu nyeupe ya ndani, kati ya nyama na ganda la nje nayo huwa na vitamini sawa kabisa na nyama ya ndani. Sharubati ya machungwa ndiyo bidhaa kuu kuliko zote ya machungwa. Huweza kuzalishwa kwa matumizi ya nyumbani lakini hasa hufanywa kwa minajili ya biashara.

Sharubati ya kugandishwa ya machungwa hutengenezwa kutokana na majimaji ya machungwa pia. Mafuta ya machungwa ni bidhaa ndogo inayotengenezwa kwa kukamua maganda ya machungwa. Hutumika kwa kuongeza ladha ya chakula na zaidi kwenye utengenezaji wa manukato.

Maua ya machungwa nayo hupendwa kwa harufu yake nzuri na hutumika mara nyingi nyakati za harusi na huhusishwa na bahati njema. Majani ya michungwa yanaweza kutumika kutengenezea chai.

Licha ya kwamba zao hili hufahamika duniani kutokana na mahitaji yake, lakini bado halijapewa kipaumbele nchini hasa kutokana na wakulima kutokuwa na uhakika wa soko kwa ajili ya bidhaa zao.

Serikali inahitajika kuwafikiria na kuwapa mbinu za kuweza kuboresha kilimo chao ili waweze kuvuna matunda mengi yanayohitajika. Ni wazi kwamba kuna wakulima wachache ambao wamepata fursa ya kufanya kazi na kampuni mbalimbali ambazo hutengeneza bidhaa za matunda, hao ndio wanaonufaika.

Lakini pia wapo ambao wana moyo ya kulima machungwa kwa wingi lakini wanaendelea kukandamizwa na wafanyabiashara wakubwa ambao huwanunuza katika mashamba. Wakulima wengi hawana vikundi vya ushirika kwani wengi hufanya kazi kwa kujitegemea.

Hiyo ni changamoto kubwa inayomfanya aendelee kukandamizwa na mfanyabiashara mkubwa. Wangekuwa na vikundi ni wazi kwamba hata bei wangejipangia wenyewe na wangekuwa na uwezo wa kusafirisha sokoni na kuuzwa kwa bei wanayotaka.

Machungwa huoza haraka. Wakati mwingine wakulima wanapata hasara kubwa hasa pale ambapo wanasubiri usafiri wa kupeleka bidhaa zao sokoni, kuna maeneo mengine barabara sio nzuri, hivyo mpaka yafike sokoni mengi yanakuwa yameoza.

Bado hawana uelewa wa kutosha ni kwa jinsi watahifadhi matunda yao yasiweze kuharibika mapema. Hiyo ni changamoto kubwa inayowakumba wakulima na wafanyabiashara wa machungwa. Kwani baadhi yao wamekuwa wakihifadhi ilimradi wanavyojua wao.

Pia, wafanyabiashara na wakulima wa machungwa hupenda kurundikana sehemu moja wakati wa msimu wa machungwa hivyo pia, biashara kuwa ngumu kwa vile wanauza kiushindani. Zipo sehemu nyingi ambazo wanaweza kufanya biashara zao na zikatoka.

Hufahamika kuwa, siku zote mazao ya mboga na matunda yana thamani kubwa kuliko mazao mengine na yanahitaji uangalifu mkubwa zaidi wakati wa uzalishaji. Udhibiti wa visumbufu vya mazao hayo wakati yakiwa shambani ni muhimu ufanyike kwa wakati unaotakiwa na kwa ufanisi ili kuleta matokeo mazuri katika uzalishaji.

Mazao ya matunda yaliyo machache na hafifu kutokana na uzalishaji duni huwa na faida ndogo ambayo inakatisha tama katika kuwekeza wakati wa kutumia teknolojia za utunzaji bora na usindikaji na hifadhi.

Ili kupata mazao bora na kupunguza uharibifu, mkulima hana budi kuzingatia kanuni za kilimo bora cha matunda pamoja na mbinu bora za uvunaji, utayarishaji na uhifadhi. Mbinu hizi zinahusisha pia usindikaji wa mazao hayo wenye lengo la kuongeza ubora na kuhifadhi kwa muda mrefu kwa ajili ya masoko na kuwezesha upatikanaji wakati wote.

(Makala kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la Habari Leo Agosti 2, 2011)

1 comment:

  1. Kaka nimekusoma, sikujua kama uko pande hizi pia khaaaa

    Papaa

    ReplyDelete