Sunday, October 9, 2011

Muziki wa Injili isiwe Biashara - Ency Mwalukasa

"NYIMBO na muziki wa Injili ni wito na si biashara kama watu wanavyofikiria.

"Waimbaji wa nyimbo za injili tuimbe nyimbo kwa wito na si kwa ajili ya kutaka kutafuta pesa au kugeuza wito huo kama ajira.

"Waimbaji wengi siku hizi hawaimbi kwa kuwa wanapenda au wanataka kumtukuza Mungu, ila wanafanya hivyo kwa ajili ya kutimiza maslahi yao binafsi."

Hivyo ndivyo anavyoanza simulizi lake, msanii Ency Mwalukasa, mama wa familia ya watoto watatu ambaye pia ni mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili nchini ambaye pia ni miongoni mwa wasanii wanaotamba kwa sanaa hiyo.Msanii huyu ambaye ana asili ya Mkoa wa Mbeya, kwa sasa anaishi jijini Dar es Salaam akiwa na na familia yake.Anasema ameamua kujishughulisha na uimbaji ambao unaambatana na kulisambaza neno la Mungu kwa njia ya sanaa ya uimbaji.

Mwanadada huyo anaeleza kuwa alianza kuzama katika usanii tangu akiwa Shule ya Msingi Sisimba iliyoko Mbeya na baadae katika Shule ya Sekondari Mbeya alikosoma na kuhitimu kidato cha nne.Anasimulia kuwa baada ya elimu ya kdato cha nne alifaulu vizuri na kuwa kati ya wale waliochaguliwa kwa ajili ya kujiunga na kidato cha tano ambako alipangiwa Shule ya Sekondari Jangwani ambako alisoma hadi kidato cha sita.Akiwa Jangwani, msanii huyo anaeleza kuwa nako alifanya vizuri katika mtihani wake wa kidato cha sita na baadaye kujiunga na chuo cha kompyuta kilichopo nchini Zambia kiitwacho Legacy Computer Institute ambako alisoma kwa muda wa mwaka mmoja na kuhitimu masomo hayo.

Baadaye, mwaka 1992-1994, Mwalukasa alifanya kazi katika mashirika mbalimbali, ingawa ilikuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, akiwa katika shirika la kidini na African Evangelistic Enterprise.Shirika hilo, Mwalukasa anasema lilikuwa likijihusisha na masuala ya huduma za kiroho na usambazaji wa neno la Mungu katika sehemu mbalimbali za Afrika.Baada ya kutoka katika shirika hilo, alijiunga na shirika jingine liitwalo Mission Aviation Fellowship(MAF) kwa muda wa miaka miwili na baada ya hapo alijiunga na El Akiwa katika shirika hilo la MAF, mwanamama huyo anasema kuwa akishughulika na shughuli za utoaji wa huduma ya neno la Mungu katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania.

Mwanamama huyo anasema kuwa baada ya kufanya kazi katika mashirika yote hayo, ndipo akaamua kufundisha dini katika shule mbalimbali . Huko alifundisha dini na maadili mema, wakati huo akiwa chini ya shirika la Scripture Union ambako alifanya kazi kwa muda wa miaka mitano.

Kwanini aliamua kufanya kazi katika mashirika ya dini?

Anajibu kuwa ni kutokana na jinsi alivyokuwa akiipenda dini na hadi leo anaamini kuwa yeye ni kati ya watu wachache ambao wameteuliwa kufanya kazi ya kumtukuza Mungu."Hata siku moja sijutii kazi nayo ninayoifanya ambayo ni ya wito, kwani najisikia furaha na mwenye amani kila ninapoifanya kazi hii.

"Sikuchagua kazi hizi kwa kuwa sikuwa na uwezo wa kufanya kazi nyingine, nasema uwezo ninao, tena sana, lakini napenda kumtukuza Mungu,"anasema.Anasema kuwa siku zote amekuwa akiamini kazi hiyo anayoifanya ina uwezo wa kuwasaidia watu wengi, ingawa si kwa kuwasaidia kifedha kama wanavyodhani au kutaka watu wengi, bali inaweza kuwasaidia kiroho zaidi.Anashukuru kuona kuwa kazi yake imewasaidia watu wengi, hasa kwa kuweza kuwabadilisha maisha yao, kiroho zaidi na kuwaondoa katika mazoea na tabia mbaya.

"Wapo watu ambao hutoa msaada wao kwa njia ya pesa na mali, lakini mimi nimeamua kutoa msaada huo kwa njia ya kuwakomboa watu kupitia neno la Mungu na nina furaha sana kuona angalau nimefanikiwa,"anasema kwa furaha mwanamama huyu.Lakini, pamoja na kufanya kazi zake za kila siku, anasema kuwa alikuwa akiendelea na kazi ya kuimba akiwa mwimbaji binafsi (solo artist). Anaongeza kwamba siku zote alikuwa akipenda sana kuimba, hasa nyimbo za Injili.

Tangu azame katika fani hiyo, Ency anasema kuwa ameshiriki kutunga na kuimba nyimbo nyingi akiwa ametunga nyimbo nyingi.Anazitaja baadhi yake kuwa ni, Tanzania ni nchi yetu,Tanzania njoo kwa Bwana,Hapo mwanzo neno moja na nyingine nyingi ambazo zinahamasisha watu kutambua uwezo wa Mungu katika kusaidia watu wake.

Anasema kuwa kila siku, yeye hufurahi kuona shughuli yake anayofanya ya uimbaji wa nyimbo za Injili inakua na kupata umaarufu.Anaongeza kuwa siku zote amekuwa akipenda sana kumtukuza Mungu na kuamini kuwa ndiye msaidizi wake katika karibu kila jambo, kwani anaamini kila alifanyalo ni kwa uwezo wa Mungu na hakuna atakaloweza kulifanya bila msaada wake (Mungu).

"Si kama nilishindwa kwenda kufanya kazi nyingine zozote. La hasha! Uwezo na akili nikiwa shuleni nilikuwa nao na hadi sasa ninao na ningeweza kusoma somo lolote na nikafaulu, ila kazi ninayoifanya ni ya wito zaidi, "anasema.Anasimulia kuwa akiwa shuleni sikuzote alikuwa anao uwezo sana darasani kimasomo na ndio maana aliweza kufaulu masomo yake tangu shule ya msingi hadi chuo na kama angetaka angeweza kujiendeleza zaidi kimasomo."Laiti ningetaka ningejiendeleza kwa masomo mengine kama ya uhasibu, udaktari na mengineyo, lakini nikaamua kujielekeza zaidi katika kumtukuza Mungu," anaeleza.

Anaongeza kuwa amekuwa akiamini kuwa binadamu awapo duniani ni vizuri kujitahidi kufanya kazi yoyote au kitu ambacho moyo wako unakipenda na kamwe asifanye kazi kwa kuwa eti fulani anaifanya.Kwa hilo, msanii na mwanamama huyo anasema itakuwa sawa na kuunyayasa moyo wako na kutoutenda haki, pengine hata mbele za mwokozi.Anasema kuwa na ndoto yake na kutaka kuitimiza kumechangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikiwa kwake. Anawashukuru wazazi wake kwa kumruhusu kufikia azma yake, hasa baada ya kuchagua kazi ya kufanya.

Anawashauri wazazi wawasimamie watoto wao katika kuchagua aina ya kazi za kufanya, isipokuwa wawape uhuru wa kuchagua nini wanataka kusomea au kufanya kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.Hata hivyo, anaeleza mshangao wake hasa kwa baadhi ya watu, hasa akinamama ambao wanadiriki kufanya vitu ambavyo hawana uwezo navyo. Anaeleza kuwa kutokana na baadhi yao kuiga kwa ajili siyo ya kufanikiwa, au kwa sababu tu fulani anafanya hivyo, imesababisha wengi wao kushindwa kufanikiwa.Anakiri hata hivyo kwamba kila mtu duniani ana wito wake wa kufanya kitu, lakini kama mtu atakuwa anapenda kufanya vitu kwa kuiga au kwa vile wanafanya hivyo wengine, si vizuri.Hadhani kuwa hilo linafanyika kwa kwa ajili ya kujiletea maendeleo, akiamini kuwa kila siku mtu akitaka maendeleo hapaswi kulazimisha kitu kwa nguvu.

"Kwa watu wanofanya biashara usione mwenzako anafanya biashara hata za mamilioni ya fedha nawe ukataka kufanya hizo hizo biashara, angalia kwanza unao uwezo katika biashara na kama huwezi basi fanya kitu kitu kingine kulingana na uwezo wako na maendeleo yatakuja taratibu,"anashauri.Msanii huyo anasema kuwa ndiyo maana anashiriki kazi ya muziki huu wa Injili, siku zote akiamini kuwa ndiyo kazi ya wito wake na kamwe hafikirii kuiacha au kujiondoa.Hata hivyo, anasema kuwa hapendi tabia ya wasanii na waimbaji wengine kuchukulia uimbaji huo wa nyimbo na tungo za dini kama moja ya sehemu ya ajira tu, jambo ambalo anaamini kuwa huenda ikasababisha nyimbo hizo za injili kukosa thamani. Pia, jambo hilo halileti picha nzuri, hasa ikizingatiwa kuwa Injili ni neno la Mungu."Unajua watu wanashindwa kuelewa kuwa uimbaji ni wito na si biashara kama wafanyavyo wengine na pia ni dhambi kuifanya Injili kuwa kitegauchumi, bila kuiishi na kutegemea kuchuma tukupitia nyimbo hizo za injili tu,"anasema.

Anaamini kuwa wapo baadhi ya wasanii ambao wana mtazamo kama huo na hao ndio wanapotosha maana halisi ya muziki huo. Kwa mtazamo wake, anasema kuwa analaani tabia kama hiyo kwa vile si tu kudhalilisha nyimbo muziki au nyimbo za injili, pia inamdhalilisha hata mwimbaji mwenyewe.Anasema kuwa haileti picha nzuri kwa mfano mtu unapokutana na mwimbaji wa nyimbo za injili au hata kumwona akiwa yupo katika mazingira mabaya na pia katika mavazi yasiyo na muonekano mzuri mbele za watu."Nashauri kwamba uimbaji huu wa muziku wa Injili usiishie tu katika burudani, bali uimbaji huu uwe kwa lengo la kutangaza neno la Mungu na watu waweze kubadilika kwa kupitia uimbaji huu," anaonya.Anaongeza kuwa kitu cha kushangaza hasa siku hizi ni kuona nyimbo za Injili zimekuwa ni kama sehemu ya burudani na kuwakuta watu wanaburudika nazo na kisha kuacha hapo hapo, kitu ambacho anasema kuwa si lengo la muziki huo, ambao unajielekeza zaidi katika kusaidia watu watu kubadilika kupitia sanaa hiyo iliyomo katika neno la Mungu.

Anasema kuwa yeye anapokuwa anaimba nyimbo jukwaani, kwake nyimbo hizo za Injili, lengo lake si kuwaelekeza watu kaitka kupata burudani na kisha kuondoka, bali ni kwa lengo la watu kupata ujumbe,kuelewa na kisha kuufanyia kazi kwa kujua ni nini wanatakiwa wafanye.Mwanamama huyo ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Woman of Wisdom Trust Fund, shirika linalojihusha na kuwasaidia watoto yatima na wasio jiweza anasema jamii inatakiwa kuwajali watu hao.Anasema kuwa kikundi chake hicho kinasaidia watoto 20 wanaosaidiwa kwa kusomeshwa na pia kupata mahitaji mengine katika maisha. Ili kutimiza azma hiyo, Mwalukasa anasema wamekuwa wakiandaa matamasha mbalimbali kwa ajili ya kusaidia watu wasiojiweza.

Kwa upande wa kazi yake, hivi karibuni alizindua albamu yake ijulikanayo kama, Nakuhimidi ambayo aliizindua katika ukumbi wa Land Mark Hotel , Ubungo jijini Dar es Salaam. Anakiri kuwa uzinduzi huo ulikuwa wa aina yake baada ya kuhudhuriwa na watu wa rika tofauti tofauti.Anasema kuwa fedha zilizopatikana kutokana na tamasha hilo zilitengwa kwa ajili ya kusaidia watu wasiojiweza na yatima ambao ndio walengwa katika mfuko wake.Anaamini kuwa Watanzania ni watu wenye upendo na umoja, hivyo ni lazima waweze kuonyesha upendo huo kwa watu hasa wale wanohitaji msaada kwa kuwapatia msaada hata kama ni mdogo.

Anasema kuwa kutoa msaada kwa wasiojiweza haimaaanishi uwe na uwezo mkubwa kwani hata kama una uwezo mdogo, mtu anaweza kuonyesha upendo huo kwa kutoa msaada kulingana na uwezo. "Tatizo watu wameweka fikra kwamba wasiojiweza wanatakiwa kusaidiwa na mashirika tu kitu ambacho si cha kweli kwani hata mtu mbinafsi unaweza kuonyesha upendo wako kwa kuwasaidia watu hawa,"anasema.Anakariri usemi wa wahenga usemao, 'kutoa ni moyo na si utajiri' na kuongeza kuwa umefika wakati kwa kila Mtanzania kutoa ushirikiano kwa watu hao ambao maisha yao yanawategemea wengine."Binafsi huwa inaniuma sana nikipita barabarani au mitaani, nikakutana na watoto wadogo wakiomba, hawa hawana mtu wa kuwasaidia na wakati huohuo wapo watoto wa umri kama wao hawako shuleni, jamani tuwasaidie,"anamalizia.


[Makala hii ni kwa mujibu wa mtandao wa  Habari Tanzania]

No comments:

Post a Comment